TAMKO LA KANISA LA AICT KUHUSU KUKAMATWA KWA WAFANYAKAZI WA HOSPITALI TEULE YA KOLANDOTO

Hivi karibuni, gazeti moja litolewalo mara moja kwa juma hapa nchini lilichapisha habari juu ya kushikiliwa na TAKUKURU kwa watumishi watatu wa Hospitari Teule ya Kolandoto iliyoko Shinyanga. Hospitali hii, ambayo ni ya kanisa la Africa Inland Church, Tanzania, ilifunguliwa mwaka 1913 na baadaye mwaka 1950 ilianzisha mafunzo ya Ukunga.

Mwaka 2013 kanisa liliingia mkataba na serikali na kuifanya Hospitali ya Kolandoto kuwa ni Hospitali Teule na hivyo kuweza kupata ruzuku ya serkali. Mwezi Mei mwaka huu watumishi watatu wa hospitali hiyo walishikiliwa na TAKUKURU baada ya tasisi hiyo kufanya ukaguzi hapo hospitalini. Siku moja baada ya watumishi hao kukamatwa, Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Askofu Silas Kezakubi, pamoja na Katibu wake Mkuu, Mchungaji Zakayo Bugota walifika Kolandoto ili kufahamu chanzo cha kukamatwa kwa watumishi hao. Kutokana na vikao ilibainika kuwa chanzo cha kushikiliwa kwa watumishi hao ilikuwa ni ukaguzi uliofanywa na taasisi hiyo ya fedha za ruzuku kutoka serikalini.

 Kwa kuwa kanisa halina njia ya kupata taarifa za taasisi ya serikali, Askofu Mkuu, kwanza, aliiomba Kamisheni ya Kikristo – Christian Social Services Commission (CSSC) ambayo ndiyo mratibu wa mikata yote ya namna hii kati ya serikali na makanisa, wapate kuuangalia mkataba wa ushirikiano huo umesema nini linapotokea jambo la namna hii na kufanya mawasiliano na viongozi husika serikalini na kulipa kanisa taarifa. Pili, Askofu Mkuu aliagiza Mkaguzi wa ndani wa kanisa aende Kolandoto mara moja kufanya ukaguzi, na hasa juu ya matumizi ya fedha husika na kuleta taarifa.  Taarifa hizo zote zitakapokamilika na kufikishwa Makao Makuu ya kanisa ndipo kanisa la Africa Inland Tanzania litakuwa na kitu cha kuzungumza. Kwa hivi sasa kanisa bado halijatoa kauli juu ya jambo hili.

You must sign in to comment.Click Here to Sign In or Here to Register
Comments
    No comments found