AZIMIO LA BARAZA LA UTENDAJI LA SINODI KUU YA AICT DHIDI YA WATUMISHI WA KANISA WALIOPELEKEA KUUZWA KWA SHULE YA SEKONDARI YA ASKOFU NKOLA (BISHOP NKOLA SECONDARY SCHOOL)

Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT Tanzania, Silas M. Kezakubi akiwa anatoa taarifa ya baraza la utendaji la sinodi kuu ya AICT katika kanisa la Kambarage Shinyanga, leo asubuhi.


Katika kikao chake cha dharura kilichofanyika Makongoro, Mwanza Machi 8, 2017 kufuatia kuuzwa kwa Shule ya Sekondari ya Askofu Nkola (Bishop Nkola Secondary School), Baraza la Utendaji la Sinodi Kuu ya AICT liliunda Tume Huru kuchunguza sababu na mazingira yaliyopelekea hasara na upotevu wa mali hiyo isiyoondosheka na hivyo kuleta aibu kubwa kwa kanisa. Shule hiyo ya kanisa iliuzwa kwa njia ya Mnada mnamo Februari 23, 2017 baada ya Dayosisi hiyo ya Shinyanga kushindwa kurejesha CRDB mkopo wa kiasi cha TZS 400,000,000.00 (Milioni Mia Nne) ambao shule hiyo iliwekwa kama dhamana.

Tume Huru ilifika Shinyanga na kufanya uchunguzi wake Machi 16-20, 2017 na kukabidhi Taarifa yake kwa Askofu Mkuu wa AICT Machi 27, 2017.

Katika kikao chake cha kawaida kilichofanyika Makongoro, Mwanza Machi 30-31, 2017 Baraza la Utendaji la Sinodi Kuu, pamoja na masuala mengine, lilipokea Taarifa ya Tume Huru na kujadili kwa kina maelezo na mapendekezo yote yaliyowasilishwa kwa marefu na mapana. Wajumbe wa Baraza la Utendaji la Sinodi Kuu waliridhika na taarifa na hiyo walichukua hatua kali kwa watumishi wa kanisa wote wa AICT Dayosisi ya Shinyanga waliokuwapo wakati wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Askofu Nkola (Bishop Nkola Secondary School) na wale waliopo sasa kwa matumizi mabaya ya madaraka na fedha ya Africa Inland Church Tanzania (AICT). Mambo hayo ndiyo yalipelekea shule hiyo kuuzwa.

  1. Baraza la Utendaji la Sinodi Kuu kwa mujibu wa Katiba ya AICT Ibara ya 23 (3) lilimtaka Askofu John Kanoni Nkola kustaafu mara moja. Yeye alishindwa kuwasimamia watendaji wake na pia hakuweza kupeleka taarifa mapema kwenye mabaraza ya juu.
  2. Baraza la Utendaji la Sinodi Kuu kwa mujibu wa Katiba ya AICT Ibara ya 23 (3) lilimtaka Askofu John Bunango aliyekuwa Katibu Mkuu wa AICT Dayosisi ya Shinyanga wakati wa kukopa na kutumia fedha hizo kujiuzuru. Akiwa Katibu Mkuu wakati wa kukopa na kutumia fedha hizo, alijihusisha na matumizi mabaya ya madaraka na matumizi mabaya ya fedha.
  3. Baraza la Utendaji la Sinodi Kuu kwa mujibu wa Sheria I (a) lilimwondoa katika kazi ya Uchungaji Mchungaji Mapambano Jacob, Katibu Mkuu wa AICT Dayosisi ya Shinyanga wakati Shule inauzwa. Yeye alihusika na matumizi mabaya ya madaraka na fedha za shule.
  4. Baraza la Utendaji la Sinodi Kuu kwa mujibu wa Katiba ya AICT Sheria I (a) lilimwondoa katika kazi ya Uchungaji Mchungaji Emmanueli Petro Isaya ambaye alijihusisha na matumizi mabaya wakati wa ujenzi wa shule hiyo.
  5. Baraza la Utendaji la Sinodi Kuu kwa mujibu wa Katiba ya AICT Sheria I (a) lilimwondoa katika kazi ya Uchungaji Mchungaji Meshaka Kulwa ambaye alijihusisha na matumizi mabaya ya fedha za mkopo huo.

Baraza la Utendaji la Sinodi Kuu liliagiza ukaguzi wa ndani ufanyike haraka na kubaini wale ambao wamechukua mali ya kanisa kuirudisha haraka na pia wachukuliwe hatua.

Pamoja na hatua hizo Baraza la Utendaji limemshauri Askofu Mkuu kuita kikao cha dharura cha Sinodi Kuu ya AICT siku ya Ijumaa Aprili 28, 2017 kutoa uamuzi wa mwisho dhidi ya Askofu John Kanoni Nkola pamoja na Askofu John Bunango.

You must sign in to comment.Click Here to Sign In or Here to Register
Comments
    No comments found