KUUZWA KWA BISHOP NKOLA SECONDARY SCHOOL, SINODI KUU YARIDHIA MAAMUZI YA BARAZA LA UTENDAJI

Sinodi Kuu ya Africa Inland Church Tanzania, imeridhia kuwaondoa uaskofu Askofu John Kanoni Nkola na Askofu John Bunango. Sinodi hiyo, ambayo ilihudhuliwa na wawakilishi wapatao 800 kutoka nchini kote, ilipokea taarifa ya Baraza la Utendaji la kanisa  iliyotolewa na Askofu Mkuu Silas Kezakubi ambayo ilitaka maaskofu hao waondolewe uaskofu kutokana na kuhusika kwao katika matumizi mabaya ya madaraka na ubadhilifu wa Shilingi milioni 400 za mkopo wa benki ya CRDB.

Sakata hili lilianza tarehe 22 February, 2017 pale Shule ya Sekondari ya Bishop Nkola ilipopigwa mnada na benki ya CRDB kutokana na deni hilo. Shule hiyo, ambayo ilijengwa mwaka 2006 kwa michango ya wakristo pamoja na harambee iliyoongozwa na Waziri Mkuu wakati huo, Mheshimiwa Fredrick Sumaye, iliwekwa kwa dhamana na uongozi wa Dayosisi ya Shinyanga ili kupata mkopo wa milioni 400/= wa kuiboresha. Baada ya kuuzwa kwa shule hiyo kwa njia ya mnada, Askofu Mkuu aliitisha kikao cha Utendaji cha dharura ili kujadiri jambo hilo. Kikao hicho kiliteua Tume Huru ya kufanya uchunguzi ili kubaini sababu zilizopelekea shule hiyo ishindwe kulipa mkopo huo hata ipigwe mnada.

Tume Huru ilitoa taarifaya yake katika Baraza la Utendaji la tarehe 30 March 2017. Taarifa hiyo ilibainisha ubadhilifu uliofanywa na viongozi pamoja na watendaji wa Dayosisi ya Shinyanga wa wakati huo juu ya mkopo huo. Ikielezea hali iliyokuwepo, taarifa hiyo inasema, “Hata hivyo, mfumo mzima wa Ofisi ya Uaskofu ya AIC Dayosisi ya Shinyanga ni kama walimwacha Yesu walipopokea mkopo wa Shilingi 400,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa shule, wakatamani kujitajirisha ghafla”.

Ubadhilifu na kukosa uaminifu kulipelekea miundombinu yote iliyokuwa imepangwa kujengwa isikamilike na tena ijengwe kwa ubora wa chini sana. Kutokana na hayo, badala ya kuingiza wanafunzi wengi na kupata mapato mengi ili kulipa deni la CRDB, shule ilizidi kudidimia.

Katika maamuzi yake hapo tarehe 31 March, 2017, Baraza la Utendaji liliwachukulia hatua wote waliohusika na mkopo huo. Kwa mjibu wa Katiba ya kanisa, Baraza liliwavua uchungaji Mchungaji Mapambano Jacob (Katibu Mkuu wa sasa) Mchungaji Meshack Kulwa (ambaye alihusika kusimamia ujenzi wa uzio) na Mchungaji Emmanuel Isaya (ambaye alikuwa katibu wa elimu). Kwa mjibu wa katiba pia Baraza lilimwomba Askofu Dr John Nkola kustaafu na Askofu John Bunango aliombwa kujiuzuru.

Kwa kufuata Katiba ya kanisa, Askofu anaondolewa na Sinodi kuu baada ya kuombwa kustaafu au kujiuzuru na Baraza la Utendaji. Hivyo, Sinodi kuu iliyokutana Makongoro Mwanza tarehe 28 April, iliridhia kuwaondoa uaskofu hao wawili.

 

You must sign in to comment.Click Here to Sign In or Here to Register
Comments
    No comments found